Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amesema ili mahakama maalum
ya mafisadi ifanye kazi kwa ufanisi, inapaswa Polisi na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ziimarishwe.
Jaji Warioba alisema hayo jana jijini Dar es Salaam, baada ya
kufanya mazungumzo na Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison
Mwakyembe, ofisini kwake.
Warioba ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
alisema suala la kuanzishwa kwa mahakama hiyo ni jambo zuri lakini
kunahitajika vyombvo ambavyo vitafanya kazi na mahakama hiyo,
viimarishwe.
“Ni jambo zuri kuanzisha mahakama ya mafisadi, lakini chombo kimoja
hakiwezi kushughulikia suala hili pekee yake. Kunahitajika vyombo kama
Polisi na Takukuru ambavyo vitafanya kazi na mahakama hii viimarishwe,”
alisema.
Warioba alisema kimsingi serikali ya awamu ya tano imeanza kazi
vizuri katika kupambana na ufisadi na kufanikiwa kukusanya kodi, hivyo
ni jukumu la kila mwananchi kushirikiana na serikali ili kufanikisha
kazi hiyo.
Naye Dk. Mwakyembe alisema wizara yake imejiwekea utaratibu wa
kuwaalika viongozi wote waliowahi kuwa mawaziri katika wizara hiyo
kufanya mazungumzo nao na kutoa ushauri wa kuboresha wizara hiyo.
Dk. Mwakyembe alisema mchakato wa kuanzisha mahakama ya mafisadi
unaendelea na kwamba serikali ya awamu ya tano imejipanga kuhakikisha
tatizo la ufisadi linakomeshwa na watuhumiwa watashughulikiwa na
mahakama hiyo.
Jaji Warioba, ambaye alikuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa
Rais mwaka 1985 hadi 1990, aliwahi kuwa Waziri wa Sheria mwanzoni mwa
miaka ya 1980. Pia aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katikati ya
mika ya 1970 hadi 1985.