MWILI wa marehemu Andrew Daffa aliyefariki dunia Jumatano ya wiki
iliyopita katika Hospitali ya Amana Dar es Salaam, umezikwa juzi katika
makaburi ya Yombo Vituka chini ya ulinzi wa Polisi huku ndugu wa
marehemu wakisusa msiba huo.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mahakama ya Wilaya ya Ilala, kutupilia
mbali maombi ya ndugu wa marehemu ya kutaka kuzikwa kwa Daffa mkoani
Tanga badala ya Dar es Salaam kama alivyoomba mke wa marehemu huyo,
Glory Charles.
Aidha, kuwepo kwa ulinzi huo ni kutokana na ndugu wa upande wa
mwanamume kuweka zuio mahakamani kuomba kibali cha kupewa mwili huo kwa
ajili ya kuuzika mkoani Tanga.
Hata hivyo, mwili huo ulizikwa katika makaburi hayo ya Yombo Vituka
baada ya misa iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT) Usharika wa Tandika wilayani Temeke.
Awali, Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo Adelf Sachore, alisema kuwa
mahakama imeamua kuwa mwili wa marehemu huyo uzikwe eneo walikozikwa
watoto wao watano.
Hakimu Sachore alisema Wakili wa utetezi kwa upande wa mdai Daniel
Buma alidai kwamba marehemu akazikwe mkoani Tanga kwa madai mila na
desturi zao lazima mtu akifa azikwe kwao.
Alisema mtoa hoja alidai marehemu asizikwe hapa kwani hana makazi ya
kudumu ambapo katika kutoa maelezo yake hata huko Tanga hana makazi kwa
kuwa hajajenga. Mlalamikiwa pia alitoa vielelezo vyake mahakamani hapo
na kupokewa ambavyo ni cheti cha ndoa pamoja na picha za marehemu,
watoto wao na vyeti vya watoto wa marehemu ambao anaishi nao.