Msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi amevitaka vyama vya siasa kurekebisha katiba zao kwenye kipengele kinachoruhusu kuanzishwa kwa vikosi vya ulinzi na usalama.
Msajili wa vyama vya siasa nchibni, Jaji Francis Mtungi
Vyama vyenye vikosi cha ulinzi na usalama ni Chadema
chenye Red Brigade, CCM (Green Guard), CUF (Blue Guard) na sasa ACT-Wazalendo
(ACT Amani).
Mutungi alisema uanzishwaji wa vikundi hivyo
unakwenda kinyume na Katiba ya nchi inayolipa jeshi la polisi mamlaka ya
kulinda usalama wa raia na mali zao.
Akizungumza baada ya mkutano wake na vyama hivyo
jana, Jaji Mutungi alisema katiba za vyama vingi vilivyosajiliwa kabla
hajaingia ofisini vilikuwa na kifungu kinachoruhusu kuanzishwa kwa vikosi vya
ulinzi na usalama wa mali za chama au viongozi wao wawapo katika mikutano.
“Haturuhusu kifungu hicho kuwapo kwenye katiba za
vyama vinavyosajiliwa sasa (hakugusia ACT - Wazalendo). Hatuvifundishi vyama
vya siasa namna ya kuandaa katiba zao lakini tunasimamia kifungu hiki kwa vile
kinapingana na sheria.”
Jaji Mutungi alisisitiza kuwa vyama vya siasa
nchini havina uelewa wa sheria ya vyama vya siasa ambayo ndiyo inayovisimamia,
ndiyo maana vinashindwa kuendesha shughuli zao kwa mujibu wa sheria hiyo.
Kauli ya polisi
Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Ernest
Mangu alisema watapambana na vikundi vya ulinzi na usalama ndani ya vyama vya
siasa wakati wa Uchaguzi Mkuu endapo vitaingilia majukumu ya jeshi la polisi.
Alisema uanzishwaji wa vikundi hivyo ni kinyume
cha sheria inayolipa Jeshi la Polisi dhamana ya kulinda usalama wa raia na mali
zao.
Alisema vikundi hivi vilianzishwa kama chipukizi
au halaiki lakini baadaye vilikuwa na kubadili malengo na kuanza kuingilia
majukumu ya polisi na kuhatarisha amani.
Maoni ya wadau
Hata hivyo, kauli za Msajili na Mangu zilipokewa
kwa hisia tofauti na viongozi wa vyama hivyo na baadhi vikiweka wazi kuwa
havipo tayari kuachana na vikundi hivyo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM – Zanzibar, Vuai Ali
Vuai alisema vijana wa Green Guard hawaandaliwi kijeshi na kuwa tishio kama
vyama vingine, bali kuwafanya wawe vijana bora, wakakamavu na kuwajengea
uzalendo ndani ya nchi yao.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema
chama chake hakipo tayari kuivunja Red Brigade huku akiilaumu CCM kuwa kikundi
chake cha Green Guard kimepata mafunzo ya kijeshi kikifundishwa na askari
tofauti na wao ambao wanafundishwa na raia.
Chanzo Mwananchi