Akizungumza katika maadhimisho ya wiki
ya elimu, Mjema alisema anasikitishwa na baadhi ya wazazi wanaokwepa majukumu
yao kwa kuwaruhusu watoto wao kushiriki katika vitendo hivyo na kusababisha
elimu kuporomoka.
Hata hivyo, aliwapongeza watendaji na
wadau wa elimu kwa jitihada zao za kuisaidia wilaya hiyo hadi mwaka huu kuwa ya
kwanza mkoa wa Dar es Salaam kwa kufaulisha wanafunzi zaidi ya asilimia
70 .
Maadhimisho hayo yaliyofanyika Kata ya
Kijichi yaliandaliwa pamoja na Manispaa Temeke, taasisi ya kijamii ya
Ocode na Shirika la Kimataifa la We World ambapo baadhi ya shule na
wanafunzi waliofanya vizuri walipewa zawadi.
“Haiwezekani mtoto anatoka masaa matatu
bila taarifa halafu mnakuwa kimya, muda huo ni mwingi kwa binti kuharibu
maisha yake, ngoma za vigodoro na safari za ufukweni si salama lazima
tuhakikishe tunawajibika kuwakemea,” alisema Mjema.
Alisema mwaka huu waliamua kufanya kazi
maalum kwa ajili ya kuinua kiwango cha elimu ambapo matunda yake yameonekana
baada ya ufaulu kuongezeka kwa shule za msingi na sekondari.
Alisema ufaulu kwa shule za msingi
ulikuwa asilimia 72 mwaka jana kutoka asilimia 60 mwaka 2003 na asilimia 64
kutoka chini ya asilimia 50 kwa sekondari.
“Ufaulu huu umeonyesha jinsi
tulivyoamua kuwa pamoja kati ya serikali na wadau kuhakikisha elimu yetu inakua
kwa kasi, nawapongeza na nawataka kuongeza kasi zaidi ili tuongoze ngazi ya
Taifa,” alisema.
Mratibu wa Ocode, Joseph Jackson,
alisema kwa kushirikiana na We World wametumia jumla ya Sh. milioni 655.9 kwa
ajili ya kuboresha mazingira na utendaji wa kazi ya walimu kwa shule nne za
msingi.
Alizitaja shule zilizonufaika kuwa ni
Kijichi, Bwawani, Kibondemaji na Buza.
Alisema shule hizo zimeboreshwa kwa
kukarabatiwa madarasa, mitandao ya maji, jiko kwa ajili ya kupikia chakula cha
wanafunzi pamoja na ununuzi wa madawati kwa shule hizo.
Chanzo Nipashe