Rais John Magufuli      Mbeya. Panga la Rais John Magufuli lililowakata baadhi ya makatibu wakuu na manaibu wao, lilimkuta pabaya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Paul Masanja ziarani mkoani Mbeya na Naibu Waziri, Dk Medard Kaleman.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Kaleman alimueleza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abass Kandoro ofisini kwake kuwa, katika msafara wake aliongozana na Masanja, lakini naibu katibu huyo alilazimika kuondoka alfajiri ya jana kurudi Dar es Salaam baada ya Rais kutangaza safu mpya ya makatibu wakuu na manaibu wao.
Kauli hiyo ilisababisha kicheko kwa maofisa mbalimbali wa mkoa na wilaya, lakini Kandoro aliwasihi wasifurahie kwa vile mambo hayo yanaweza kuwakuta wengi.
“Mambo haya yanashtua, hata mimi na mkuu wa wilaya na wengineo tunafanya kazi huku tukijisikilizia. Kwa hiyo mheshimiwa naibu waziri tunaomba mtuombee kwa Mungu,” alisema na kusababisha vicheko zaidi.
Katika uteuzi mpya manaibu katibu wa wizara hiyo wako wawili ambao ni Profesa James Mdoe na Dk Paulina Pallangyo.
Akizungumzia sababu ya ziara hiyo, Dk Kaleman alisema alifika mkoani hapa kukagua vyanzo vya maji yanayoingia Bonde la Usangu na hatimaye kuingia kwenye mto Ruaha unaozalisha umeme wa Mtera, ili aweze kutoa maelekezo sahihi kwa viongozi wa mkoa, wilaya na vijiji.
Alisema Bwawa la Mtera ambalo lilikuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 80 za umeme kwa sasa linazalisha megawati moja hadi mbili, baada ya kukauka na kwamba, wakati umefika kwa wakazi wa mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe kuondoka kwenye vyanzo vyote vya maji.
Kwa upande wake Kandoro alisema tayari ameandika barua kwenda katika wizara hiyo kuomba kikao kitakachohusisha wizara za Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Kilimo, Mifugo na Uvuvi; Maji pamoja na Maliasili na Utalii ili kuweka mkakati wa kuliokoa bwawa hilo.
Naibu waziri huyo jana alikwenda katika vijiji viwili vilivyoko kwenye milima ya Mporoto ambako kuna vyanzo vingi vya maji.

 
Top